Jumatano 19 Agosti 2026 - 10:08
Ayatullah Arafi katika barua kumuelekea Patriaki wa Kanisa la Kiorthodoksi la Romania asisitiza mambo ya pamoja ya kidini na umuhimu wa ushirikiano

Hawza/ Mkuu wa Hawza za Iran, katika barua aliyomwandikia Patriaki wa Kanisa la Kiorthodoksi la Romania, huku akisisitiza mambo ya pamoja ya kiitikadi, kimaadili na kiirfani kati ya Uislamu wa Kishia na Ukristo wa Kiorthodoksi, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pande mbili katika kukabiliana na mgogoro wa familia na ukosefu wa imani miongoni mwa vijana.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, Mkuu wa Hawza za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika barua aliyomwandikia Patriaki Daniel, kiongozi wa Kanisa la Kiorthodoksi la Romania, huku akirejelea mambo ya kina ya pamoja kati ya Uislamu wa Kishia na Ukristo wa Kiorthodoksi katika imani za msingi, irfani na maadili, alisisitiza umuhimu wa mwingiliano unaomlenga Mwenyezi Mungu na mazungumzo baina ya dini kama njia ya kuiokoa jamii ya wanadamu kutokana na migogoro ya kimaadili na kiroho. Barua hiyo, ambayo ilikabidhiwa na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Sadiq Amin al-Din, Mkuu wa Ofisi ya Dini na Madhehebu ya Hawza, wakati wa ziara yake mjini Bucharest, kwa Dkt. Valentin Ilie, mratibu wa mazungumzo baina ya dini wa Kanisa la Kiorthodoksi la Romania, imetangazwa kuwa mwanzo wa ushirikiano mpana kati ya Hawza na Kanisa la Kiorthodoksi la Romania.

Katika barua hiyo, iliyoandikwa kwa kurejelea aya za Qur’ani na Injili, changamoto mbili kubwa za pamoja, ambazo ni tishio dhidi ya taasisi ya familia na mgogoro wa ukosefu wa imani miongoni mwa vijana, zimepewa msisitizo. Mafundisho ya Uislamu na Ukristo wa Kiorthodoksi katika kuilinda taasisi ya familia na pia kulea vizazi vyenye imani, yametajwa kuwa urithi wa pamoja ambao unaweza kuwa msingi wa ushirikiano wa kielimu na kiutafiti. Aidha, kwa kurejelea heshima kubwa ya dini zote mbili kwa Bibi Maryam Mtakatifu (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) na watakatifu, msisitizo maalumu umetolewa juu ya umuhimu wa kuwafanya watu hawa watukufu kuwa mifano ya kuigwa kwa kizazi cha vijana.

Mkuu huyo wa Hawza, katika sehemu nyingine ya barua hiyo, alitangaza utayari kamili wa Hawza za Iran kushirikiana na Kanisa la Kiorthodoksi la Romania katika nyanja mbalimbali za kielimu na kiutafiti, kidini, kiutamaduni na kijamii. Kubadilishana walimu na watafiti katika nyanja za kielimu kama vile maadili, kuandaa makongamano ya kimataifa yanayolenga familia na mambo ya kiroho, pamoja na kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za kidini, ni miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa ya ushirikiano.

Ayatullah Arafi, mwishoni mwa barua hiyo, ameutaja ushirikiano mpana na Kanisa la Kiorthodoksi la Romania kuwa hatua yenye ufanisi kuelekea kuinua kiwango cha mambo ya kiroho na maadili katika dunia ya leo, na amemuombea Patriaki Daniel pamoja na ndugu wote Wakristo afya njema na furaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Inafaa kutajwa kwamba; Hawza za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miezi ya hivi karibuni zimeandaa mfululizo wa vikao vya kielimu na mafunzo baina ya dini, vilivyoshirikisha viongozi wa kidini na wasomi wa vyuo vikuu kutoka Iran na Romania, ambavyo vimeambatana na ushiriki wa vyuo vikuu mashuhuri na Kanisa la Kiorthodoksi la Romania.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha